CONTACT US VIA: maelezopress@yahoo.com, website: habari.go.tz or follow us on twitter @Maelezo1 also find us on facebook www.facebook.com/Habari Maelezo.

Thursday, 28 May 2015

Serikali yashauriwa kuongeza bajeti ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.

Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe. Dkt. Fenella Mukangara akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo leo bungeni mjini Dodoma.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii Mhe. Said Mtanda akiwasilisha mapendekezo ya kamati yake kuhusu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo wakati wa bajeti ya wizara hiyo leo mjini Dodoma
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bi. Sihaba Nkinga (wa tatu kutoka kushoto) akiwa na Naibu Katibu Mkuu Prof. Elisante Ole Gabriel (wa pili kutoka kushoto) wakifuatilia kwa makini bajeti ya Wizara hiyo leo mjini Dodoma
Naibu Waziri wa  Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe. Juma Nkamia akimsikiliza Mbunge wa Mbeya Mjini Mhe. Joseph Mbilinyi kwenye viwanja vya bunge leo mjini Dodoma.

PICHA ZOTE NA FATMA SALUM
  Na Abraham Nyantori
 
Serikali imeshauriwa kutenga fedha za kutosha ili kuiwezesha Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Ushauri huo umetolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii wakati wa kuwasilisha mapendekezo yake leo bungeni mjini Dodoma.

Mwenyekiti wa kamati Mhe. Said Mtanda amesema Wizara hiyo ina jukumu la kuratibu na  kusimamia maendeleo ya vijana, utamaduni, michezo na habari hivyo ikipewa fungu la kutosha itaweza kuleta mabadiliko chanya kwenye sekta hizo.

Akiwasilisha Bajeti ya Wizara yake bungeni leo Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe. Dkt. Fenella Mukangara ameliomba Bunge kuidhinisha  bajeti ya wizara hiyo ya shilingi bilioni 29.4  ambapo shilingi bilioni 5 ni kwa ajili ya maendeleo na shilingi bilioni 24.4 ni matumizi ya kawaida.

Aidha Waziri Mukangara ameeleza jitihada mbalimbali zinazofanywa na wizara yake zikiwemo kuratibu na kuwajengea vijana uwezo wa kubuni mawazo bora ya kujiajiri, kuhamasisha halmashauri kutenga asilimia 5 ya bajeti yao kuboresha mifuko ya vijana na kuhamasisha uanzishaji wa SACCOS.

Katika mwaka wa fedha uliopita wa 2014/2015, Waziri Mukangara amesema wizara yake ilitoa mafunzo kwa vijana 1550 katika kujenga dhana ya  kujiajiri, na jumla ya  shilingi bilioni 2 zilikopeshwa kwa vikundi mbalimbali vya vijana kote nchini.

Kwa upande mwingine Dkt Mukangara amesema wizara yake imekamilisha miradi kadhaa ukiwemo mradi wa Mawasiliano na kukamilisha lengo la milenia la  kubadili matumizi ya analojia kwenda dijitali, mradi huo ulikamilika mwezi Aprili mwaka huu. Miradi mingine katika mwaka wa fedha uliopita ilikuwa ni ya utafiti ukiwemo wa msamiati wa lugha za jamii, utafiti wa majina fiche 1800 ya lugha za asili.

Wizara katika mwaka huu wa fedha imeahidi kuongeza ufanisi ikiwemo kuongeza ajira kwa vijana, kulinda mazingira, kutoa habari,  kulinda mila na desturi kudumisha amani na mshikamano wa katika jamii ya watanzania.

Leo ni siku ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na Wizara ya Maliasili na Utalii ambazo zimewasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara zao na hatimaye kuruhusu Bunge kuendelea kuzijadili bajeti hizo.